SPIKA wa Bunge la Jamhuri wa
Tanzania mstaafu, Mama Anna Makinda ametoa elimu wa uongozi wa Kijinsia
kwa madiwani wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam katika warsha ya siku
moja iliyoandaliwa na TGNP Mtandao ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo
madiwani hao. Akizungumza katika warsha hiyo, Bi. Makinda alisema suala
la kuwajengea uwezo wanawake linapaswa kuanza mapema mara baada ya
kumalizika kwa uchaguzi ili kupata muda zaidi wa viongozi hao kupata
elimu stahiki, kwani mara nyingi elimu hiyo hucheleweshwa kutolewa.
“…Kimsingi muda huu tumechelewa
mikakati ya kuanza kumuwezesha kiongozi mwanamke hupaswa kuanza mara
baada ya kumalizika kwa uchaguzi hii itatusaidia hata kujipanga mapema
uongozini…,” alisema Mama Makinda akizungumza na madiwani hao.
Aliwataka wanawake wote viongozi
kuwa pamoja hasa wanapopigania masuala ya wanawake ili kwani umoja mara
zote ni nguvu na utengano ni udhaifu. Changamoto za wanawake
hazitofautiani kiitikadi za chama, rangi wala imani hivyo kuna kila
sababu ya kuungana pale wanapogombea ajenda za wanawake.
Pamoja na hayo aliwataka madiwani
wanawake kujipanga kimikakati na kutokubali kuondolewa katika nafasi za
uongozi kizembe, kwani uwezo wa kuwatumikia wananchi wanao tena wa
kiwango kikubwa kama watajipanga vizuri.
“…Hivi unakubalije mtu aliye nje
kuja kukutoa katika nafasi yako kirahisi rahisi ilhali wewe upo karibu
na wananchi, usikubali tuwaoneshe kwa vitendo tulioingia tusitoke
kirahisi bila kupenda labda tupande ngazi lakini sio kushuka,”
alisisitiza Mama Makinda.
Aidha aliwaomba kufanya kazi kwa
pamoja na ushirikiano na viongozi wa kiume kwani idadi yao ni kubwa
hivyo ushawishi pekee ndio unaweza kuongezea nguvu ajenda zao.
Alibainisha idadi ya madiwani na wabunge wa kiume ni kubwa ukilinganisha
na wao hivyo njia pekee ya wao kufanikiwa ni kujenga urafiki, ukaribu
na ushawishi kwa agenda anuai zinazobebwa na wanawake.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa
Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), Bi. Suzan Lyimo akizungumza na
madiwani hao aliwaomba kuwa kitu kimoja haswa wanapopigania masuala ya
msingi kumuwezesha mwanamke.
Alisema kama wanawake hawatakuwa
kitu kimoja hawawezi kufanikiwa katika agenda zao. Hata hivyo aliongeza
kuwa usawa wa kijinsia unapaswa kuanzia ndani ya vyama vya siasa kwani
ndipo mipango mingi ya chama upangwa kwa utekelezaji zaidi.
Post a Comment