UONGOZI wa
Benki ya Azania Limited umeridhika na namna serikali ilivyopokea mawazo
ya wadau wa sekta binafsi katika mkutano walioshiriki kuuandaa mkoani
Dodoma kwa lengo la kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuishauri serikali
katika masuala mbalimbali yahusuyo kodi.
Katika mkutano huo ulioongozwa na
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango wafanyabiashara kutoka
kampuni mbalimbali za binafsi walieleza changamoto wanazokumbana nazo na
kushauri njia muafaka za kuondokana na changamoto hizo ili kuweka
mazingira mazuri ya biashara nchini.
“Lengo letu la msingi kuwepo
katika mkutano huu ni kutaka kuhakikisha sekta binafsi zinakuwa karibu
na serikali ili kupatikane nafasi ya kuelezana yale yanayoonekana ni
kikwazo katika uwekezaji, kama inavyofahamika kazi ya benki ni kutoa
mikopo na kuwezesha kampuni kutimiza malengo yake na kumudu kulipa
kodi,” alisema Bw. Godwin Seiya
Akizungumzia hali halisi ya
kiuchumi nchini Senior manager, New ventures and Industrial facilitation
wa Benki ya Azania, Bw.Godwin Seiya alisema kodi ndiyo inayoendesha
nchi hivyo hakuna namna ambayo serikali itaruhusu ukwepaji kodi lakini
mbali ya hayo serikali imefungua milango ya majadiliano na kuwasikiliza
wafanyabiashara mambo yanayowakwaza.
“Hii ni heshima kubwa tumepewa
wafanyabiashara, katika mkutano huu kama alivyoeleza Waziri Mpango,
ndipo ambapo sehemu ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha itatengenezwa
kupitia mawazo yaliyotolewa na wajumbe,” alisema Bwana Seiya
Akihutubia wajumbe katika mkutano
huo wa siku moja, Waziri Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema
serikali haina tatizo na kubadili mfumo wa kodi kwa sababu kila siku
wanatafuta namna nzuri ya kukusanya kodi bila kuwakwaza wafanyabiashara.
“Naomba niwaeleze kuwa hata
serikali inafurahi kuwa na mikutano ya namna hii, kwa sababu tunatarajia
tutapata mapendekezo yanayotekelezeka. Katika mazingira haya
niliyoeleza ningependa kuona tunapata mfumo wa kodi utakaofungulia nguvu
ya sekta binfsi,” alisema Dkt. Mpango.
Alisisitiza kuwa kwa sasa
Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayoendelea ambayo yanajipanga kuwa
na uchumi wa kati kwa kutegemea mapato ya ndani kwa sababu wahisani
wamepunguza kutoa misaada na mikopo.
“Tukiamua kufanya kazi pamoja na
kuweka nguvu zetu kwa kusikilizana changamoto na kupata majibu mazuri;
hakuna kitakachotushinda. Katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu wa fedha
2017/18 tuliingiza mambo mengi kutokana na ushauri wa sekta binafsi.
Tutaendelea kufanya hivyo na hii ni ahadi ya serikali,” alisema Dkt.
Mpango.
Kwa upande wake mwakilishi wa
jumuiya ya wenye viwanda nchini (CTI) Dk. Samwel Nyantahe pamoja na
mambo mengine, amesisitiza umuhimu wa serikali pamoja na jumuiya ya
wafanyabiashara kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto
mbalimbali zinazojitokeza katika sekta binafsi.
“Sekta binafsi ina changamoto
nyingi tunazokabiliana nazo, tutumie vizuri fursa kama hizi za kukutana
na serikali kueleza mambo yanayotukwaza ili yapatiwe majibu, lakini pia
kama tuna ya kushauri huu ndio wakati wake,” alisema Dkt. Nyantahe.
Azania Bank Limited imeweka wazi
kuwa ushiriki wake katika maandalizi ya mkutano huo muhimu kwa sekta
binafsi na sekta ya umma ni kutaka kuongeza fursa kwa sekta binafsi
ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia ukuzaji uchumi kupitia ulipaji kodi.
Post a Comment