
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na vitendo
vya uhalifu ili kuhakikisha kuwa wakazi wa Mkoa huu wanaendelea kuwa
salama na mali zao. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea na
Oparesheni na Doria za mara kwa mara ili kudhibiti vitendo vya uhalifu
pamoja na kuzuia matukio mbalimbali yakiwemo ya uporaji na ukabaji na
kama mtakumbuka siku za karibuni kulijitokeza vikundi vya uhalifu
vilivyojiita majina ya wakorea weusi, weupe. Hata hivyo kumekuwa na
matukio mawili kama ifuatavyo:-
Mnamo 24.03.2018 majira ya saa
00.15 usiku askari Polisi waliokuwa katika doria na oparesheni ya
kukamata wahalifu huko maeneo ya Mtaa wa Airport ya Zamani, Kata ya
Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya na katika Doria hiyo
walikamatwa vijana kumi na wawili akiwemo kijana mmoja ambaye
alifahamika kwa jina la ALAIN ACHILE [22] Mkazi wa Airport ya zamani.
Mtuhumiwa huyu pamoja na
wenzake baada ya kukamatwa walifikishwa kituo kikuu cha Polisi Mbeya
Mjini na kufunguliwa mashitaka ya UZEMBE NA UKOROFI ambapo walishikiliwa
na kuhojiwa.
Mnamo 25.03.2018 majira ya saa
10.45 asubuhi mtuhumiwa ALAIN ACHILE alidhaminiwa na ndugu zake na
kwenda nyumbani kwao. Ilipofika majira ya saa 18.00 jioni zilipatikana
taarifa kuwa mtuhumiwa huyo amefariki dunia.
Mara baada ya taarifa hizo,
wananchi wa eneo hilo la Airport ya zamani hasa vijana walianza kufanya
fujo kwa kutuhumu kuwa Polisi wamehusika na kifo hicho hivyo kwenda
nyumbani kwa Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa BOAZ KAZIMOTO [74] Mkazi wa
Iyela kwa kumtuhumu kuwa yeye ndiye aliyewaita Polisi kwenda kumkamata
marehemu ALAIN ACHILE na wenzake hivyo walipofika nyumbani kwa
Mwenyekiti huyo walianza kuvunja madirisha ya nyumba yake, Baadaye
walikwenda kwenye barabara za mtaa huo na kupanga mawe barabarani na
kuchoma moto meza za wafanyabiashara wa Soko la Maendeleo.
Halikadhalika walikwenda Ofisi
ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Iyela na kubomoa milango yote, kuharibu
samani za ofisi na kuharibu baadhi ya nyaraka mbalimbali za ofisi ambazo
hadi sasa thamani yake haijajulikana. Sanjari na hayo pia walikwenda
nyumbani kwa askari aitwaye H.4325 PC YOHANA wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia na kuvunja madirisha ya nyumba yake huku wakitoa kauli ya kuwa
wataichoma moto nyumba hiyo.
Kutokana na vurugu hizo askari
walifika eneo hilo ili kutuliza vurugu hizo lakini wakati wanafika
wananchi hao walianza kurusha mawe ili kuwadhuru askari waliokwenda
eneo hilo.
Kutokana na vurugu hizo, Gari
yenye namba za usajili PT 1987 aina ya Toyota Land Cruiser Mali ya
Polisi Wilaya ya Mbeya mjini ilivunjwa kioo cha mbele kwa mawe hivyo
kulazimu askari kufyatua mabomu ya machozi kutuliza ghasia hizo.
Aidha katika vurugu hizo watuhumiwa nane [08] wamekamatwa kuhusika na vurugu hizo ambao ni:-
- ELIUD DAUD [22] Mkazi wa Iyela
- BARIKI MASUDI [30] Mkazi wa Iyela
- FRANK KILEMI [33] Mkazi wa Airport ya zamani
- KRIST NELSON [33] Mkazi wa Airport ya zamani
- ESTOM MBALO [24] Mkazi wa Airport ya zamani
- ROBERT MWANGUPILI [24] Mkazi wa Iyela
- ISSA NELSON [26] Mkazi wa Iyela
- FELIX MBILINYI [21] Mkazi wa Airport ya zamani.
Watuhumiwa hao wanahojiwa
na Jeshi la Polisi na watafikishwa Mahakamani wakati wowote mara baada
ya taratibu za kisheria zitakapokamilika. Aidha juhudi ya kuwasaka
wengine waliohusika na kuanzisha vurugu hizo zinaendelea.
Nichukue nafasi hii kuwapa
pole wazazi, ndugu na hata walioguswa na kifo cha kijana huyu,
niwathibitishie wananchi kuwa Jeshi la Polisi halikuhusika na kifo cha
kijana huyu kwa aina yoyote. Aidha nimefungua jalada la uchunguzi [PE]
kupitia Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai [RCO] ofisini
kwangu kwa ajili ya uchunguzi wa kifo cha ALLAIN ACHILE.
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WALIOINGILIA MIUNDOMBINU YA TANESCO.
Mnamo tarehe 23/03/2018 Jeshi
la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na maafisa wa Tanesco lilifanya
Oparesheni katika maeneo ya vijiji vya Isebe na Isajilo vilivyopo
Wilaya ya Rungwe kufuatia taarifa za siri toka kwa raia wema kuwa kuna
watu wanaingilia miundombinu ya Tanesco katika vijiji hivyo pamoja na
kufanya wizi wa nguzo za umeme na kuwaunganishia umeme wakazi wa maeneo
hayo kinyume cha sheria.
Katika Oparesheni hiyo,
watuhumiwa wanne [04] wamekamatwa kwa kosa la kuingilia miundombinu ya
Shirika la Umeme [Tanesco]. Watuhumiwa waliokamatwa ni:-
- IDD HAMIS MWAMBUSYE [31] Mkazi wa Bagamoyo.
- BENARD KIBONDI [40] Mkazi wa Kikota
- THOBIAS WILFRED [42] Mkazi wa Iponjola
- Eng.GEOFREY MSUNGA [30] Mkazi wa Mbeya
Aidha miongoni mwa watuhumiwa
hao baada ya kukamatwa na kupekuliwa majumbani kwao walikutwa na vifaa
mbalimbali vya umeme ambavyo ni:-
- Mita za umeme 27 aina ya Tropical
- Nyanya za umeme mkubwa na mdogo za aina mbalimbali
- Kitoboleo cha nguzo
- Stay Insulator
- Plaizi
- Tester za umeme
- Seal za mita za umeme
- Vibao vya tahadhari vinavyobandikwa kwenye nguzo za umeme
- Nguzo 57 za umeme ambazo walikuwa zikitumika kuwaunganishia umeme wananchi.
Watuhumiwa watafikishwa
Mahakamani mara tu baada ya upelelezi kukamilika. Aidha msako mkali
unaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wanaojihusisha na uhujumu wa
miundombinu ya Shirika la Umeme – TANESCO katika maeneo mbalimbali.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA anatoa wito kwa jamii
kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wafuate
taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kutii sheria bila shuruti. Aidha
anatoa wito kwa jamii kuachana na tamaa ya mali hasa kwa kujihusisha na
vitendo vya kihalifu ili wapate mali na badala yake wafanye kazi
halali.
Post a Comment